Kwa mujibu wa Kurugenzi ya Kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Muhammad Hussein Mokhtari, katika mahojiano na gazeti la Avvenire nchini Italia, alizungumzia mashambulizi yaliyofanywa na utawala haramu wa Kizayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema:
“Kitendo hiki cha utawala wa Kizayuni ni ukiukaji wa Kifungu cha 2, Ibara ya 4 ya Katiba ya Umoja wa Mataifa, na ni uvamizi wa wazi dhidi ya nchi huru ya Iran. Majibu ya Iran kutokana na uvamizi huu ni haki halali na ya kisheria kwa mujibu wa Kifungu cha 51 cha Katiba hiyo.”
Aliendelea kusema kuwa, vikosi vya kijeshi vya Iran, kwa heshima na uwezo, vinalinda ardhi ya taifa lao dhidi ya utawala huo wa kinyakuzi.
Alisema kuwa dhima ya kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa ilikuwa ni kuzuia uvamizi na kukabiliana na vitisho vya amani na utulivu wa kimataifa, na akauliza:
"Je!, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limechukua hatua yoyote kuhusiana na jambo hili? Je! Taasisi za kimataifa na mashirika ya haki za binadamu yamechukua hatua yoyote kukabiliana na mauaji ya raia wasio na hatia – wanawake na watoto – yanayofanywa waziwazi?”
Mokhtari aliongeza kuwa: "Tunatarajia viongozi wa Mji Mtakatifu wa Vatican kulaani waziwazi na kwa mujibu wa mafundisho ya kidini, kitendo hiki cha wazi cha uhalifu na uvamizi wa kinyama.”
Aliwataka viongozi wote wa kidini kuchukua hatua za kweli kukabiliana na uchokozi huu hatari, ambao umeuweka ulimwengu katika tishio kubwa lisilokuwa na mfano wa awali wa kupoteza amani na usalama wa kimataifa.
Mokhtari pia alibainisha kuwa: “Uvamizi huu usio wa kibinadamu uliofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya nchi yetu haujafanywa bila kuratibiwa; umeungwa mkono kikamilifu na Rais wa Marekani, kwa hivyo Marekani itawajibika kwa matokeo mabaya ya uchokozi huu.”
Aidha, balozi huyo aliashiria maneno ya Papa Leon wa kumi na nne, aliyesema kuwa “hakuna mtu yeyote anayepaswa kuutishia uwepo wa taifa jingine.”
Lakini sasa, alisema Mokhtari, utawala wa kigaidi wa Kizayuni, mbele ya macho ya serikali na taasisi za kimataifa, unavamia taifa huru, mwanachama wa Umoja wa Mataifa, na kuwaua makamanda wa kijeshi, wanasayansi wa nyuklia, na pia raia wasio na hatia – wanawake na watoto.
“Unyama huu unaendelea huku sheria za kimataifa zikipuuzwa kabisa, maeneo ya makazi yakishambuliwa, na baadhi ya serikali hata zikishiriki au kupongeza mashambulizi haya.
Akatamatisha kwa kusema: “Watu wengi duniani sasa wanaamini kuwa taasisi za kimataifa zimepoteza sababu ya kuwepo kwao, na zimekuwa dhaifu kushughulikia masuala ya msingi kama amani ya mataifa na kulinda mipaka ya nchi dhidi ya wavamizi.”
"Hali hii pia imeonekana wazi katika uvamizi dhidi ya Lebanon, Yemen, Syria, na mauaji ya kimbari ya watu wa Ghaza, ambapo hata misaada ya kibinadamu – hasa chakula na dawa – haikuruhusiwa kuingia.”
Maoni yako